IDHAA YA KISWAHILI | DW
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo
Matangazo
Matangazo

Habari

Habari za Ulimwengu | 31.07.2020 | 10:00

Waislam washerehekea Eid al-Adha

Waislamu ulimwenguni kote wanasherehekea sikuukuu ya Eid Al Adha ambayo itaendelea kwa siku tatu, huku mahujaji wakiwa wamefika Mina kutekeleza moja ya ibada za Hijja ya kumrushia mawe shetani. Mahujaji waliovalia mavazi meupe maalumu kwa Hijja pamoja na barakoa, walirusha mawe saba dhidi ya nguzo ambayo inatumiwa kama alama ya kumlenga shetani, huku wakiwa wameweka umbali unaostahili kutoka mtu mmoja hadi mwengine. Wasimamizi wa Hijja wamewapatia mahujaji mawe yaliyosafishwa kwa dawa ya kuuwa vijidudu, ili kuwalinda na maambukizi ya virusi vya corona. Baada ya kumrushia mawe shetani, mahujaji watarudi katika msikiti mkuu wa Makka kufanya tawafu ambayo ni ibada ya kulizunguka Kaaba. Sala ya Iddi leo imefuatiwa na kuchinja wanyama, ambapo nyama baadae hutolewa kwa jamii marafiki na wasiojiweza. Hijja ya safari hii imehudhuriwa na Waislam wachache wapatao 10,000 tu ambao ni raia wa mataifa mbalimbali waliopo nchini Saudi Arabia, tofauti na ilivyozoeleka ambapo mamilioni ya Waislamu kutoka kote ulimwenguni hukutana kwa ibada hiyo kila mwaka.

Afhanistan wakubaliana kusitisha mapigano siku tatu

Raia wa Afghanistan wamesali sala ya sikukuu ya Eid al-Adha, baada ya kuanza kwa mpango wa siku tatu wa kusitisha mapigano kati ya vikosi vya serikali na kundi la Taliban. Wengi wanatarajia kuwa makubaliano hayo ya kusitisha mapigano, yatapelekea kuanzishwa mazungumzo ya kutafuta amani na kumaliza miongo miwili ya mapigano. Hii ni mara ya tatu mapigano kusimamishwa rasmi katika takriban miaka 19 ya mapigano. Aidha watu 17 waliuawa leo kutokana na mlipuko wa bomu lilotegwa ndani ya gari, masaa machache kabla ya kuanza rasmi kwa usitishwaji huo wa mapigano. Kundi la Taliban limekana kuhusika na tukio hilo.

Wanajeshi wa Ujerumani wataziba pengo la kuondoka wanajeshi wa Marekani

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani amesema leo kwamba atafanya mazungumzo baada ya kumalizika msimu wa joto na mawaziri wa majimbo ya Ujerumani yaliyoathirika kutokana na uamuzi wa Marekani wa kuondoa wanajeshi wake wapatao 12,000 nchini humo. Annegret Kramp-Karrenbauer amesema watajadili jinsi wanajeshi wa Kijerumani watakavyoweza kuyasaidia maeneo yaliyoathirika na uamuzi huo. Ameongeza kwamba watazingatia masilahi ya Wajerumani na raia ya Ulaya, kwani maisha mazuri yanahitaji usalama. Jeshi la Marekani Jumatano lilitangaza mipango yake ya kuwaondoa wanajeshi hao, kufuatia mvutano wa muda mrefu uliokuwa ukitokota kati ya Rais Donald Trump na viongozi wa Ujerumani. Hata hivyo Marekani imesema kwamba nusu ya wanajeshi hao watabakia katika mataifa mengine ya barani Ulaya kushughulikia mvutano na Urusi.

Hong Kong huenda ikaahirisha uchaguzi

Kiongozi wa Hong Kong Carrie Lam anatarajiwa hii leo kutangaza kuahirishwa kwa uchaguzi wa bunge la mji huo wa Septemba 6, kutokana na kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya corona. Uamuzi huo utakuwa pigo kwa upande wa upinzani unaopigania demokrasia Hong Kong, ambao ulikuwa na mataumaini ya kushinda wingi wa viti bungeni. Uchaguzi huo utakuwa wa kwanza tangu China ilipotangaza sheria mpya ya usalama wa kitaifa, ambayo adhabu yake ni kifungo cha maisha jela. China imesema sheria hiyo itatumika dhidi ya kile ilichokitaja kuwa uchochezi, njama za kujitenga, ugaidi na uingiliaji kati wa mataifa ya kigeni. Serikali Kuu ya China na ya Hong Kong zimesema sheria hiyo haitotumika kukandamiza uhuru wa raia wa Hong Kong, bali inahitajika kurejesha utulivu baada ya miezi kadhaa ya maandamano ya vurugu ya mwaka jana ya kuipinga serikali.

Maandamano ya upinzani Belarus yavutia watu 34,000

Hapo jana, maelfu ya watu wameshiriki katika maandamano ya upinzani katika mji mkuu wa Belarus, Minsk, ikiwa ni takriban wiki moja kabla ya uchaguzi wa rais nchini humo. Shirika ka kutetea haki za binadamu Viasna, limesema mwanasiasa Svetlana Tikhanovskaya aliyeitisha maandamano hayo, ameitikiwa na watu wapatao elfu thelathini na nne. Ni maandamano makubwa zaidi ya upinzani kuwahi kushuhudiwa katika jamhuri hiyo ya zamani ya Kisovieti. Katika uchaguzi huo ujao, Tikhanovskaya anatarajiwa kuchuana na Rais Alexander Lukashenko aliye madarakani kwa miaka 26, na ambaye anawania muhula wake wa sita madarakani. Wasimamizi wa kimataifa mara kwa mara wamekuwa wakikosoa chaguzi za Belarus, wakisema huwa zinashindwa kufuata kanuni za demokrasia.

Uchumi wa Ufaransa umeanguka kutokana na corona

Kama ilivyo nchini Ujerumani na Marekani, Ufaransa nayo imetangaza kuporomoka kwa uchumi wake kutokana na janga la virusi vya corona. Katika robo ya pili ya mwaka, uchumi wa Ufaransa umenywea kwa asilimia 13.8 kulingana na ofisi ya takwimu ya mjini Paris. Tangu robo ya kwanza ya mwaka, kulionekana dalili za athari za janga la corona katika uchumi wa Ufaransa ambao ni wa pili kwa ukubwa katika kanda inayotumia sarafu ya euro. Hapo jana, Ujerumani imetangaza kuporomoka kwa uchumi wake kwa asilimia 10, na Marekani imeshuhudia kuanguka kwa uchumi wake kwa thuluthi moja.

Rais wa zamani wa FIFA Blatter ataka mrithi wake Infntino asimamishwe

Rais wa zamani wa shirkisho la mpira wa miguu dunini FIFA, Sepp Blatter ametoa mwito kwa mrithi wake, Gianni Infantinno kusimamishwa kazi na shirikisho hilo la dunia, baada ya kufunguliwa kwa kesi ya uhalifu dhidi ya Infatino nchini Uswisi. Mamlaka nchini Uswisi jana Alhamisi zilisema mashtaka yalifunguliwa dhidi ya mkuu huyo wa sasa wa FIFA na mwendesha mashtaka maalumu anaechunguza mikutano aliyofanya na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Uswisi Michael Lauber. Luber na Infantino wamekanusha kutenda makosa yoyote. Blatter amesema katika taarifa kwa shirika la habari la reuters, kwamba ni wazi kwamba kamati ya maadili ya FIFA inapaswa kufungua kesi dhidi ya Infantino na hivyo inapaswa kumsimamisha. Blatter mwenye alisimamishwa na baadae kupigwa marufuku na kamati ya maadili ya FIFA baada ya kushtakiwa nchini Uswisi mwaka 2015. Uchunguzi huo bado unaendelea na Blatter, ambaye anakusha kutenda kosa lolote, hajashtakiwa.

Matukio ya kisiasa

Matukio ya Afrika

Masuala ya jamii

Michezo

Habari kwa lugha ya Kiingereza

Redaktionsfoto Kisuaheli (DW/Joel Pawlak)

Bonyeza hapa kupata Matangazo na ripoti zetu

Matangazo
Tazama vidio 00:52